Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu

WCF Logo
Usajili wa Wafanyabiashara wa Mbegu
Usajili wa Wafanyabiashara wa Mbegu

Utangulizi

Mfanyabiashara wa mbegu ni yeyote yule ambaye anajishughulisha ama na uzalishaji, uchakataji, ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa mbegu au vyote kwa pamoja. Ili kuwa mfanyabiashara wa mbegu ni lazima kukidhi matakwa kama yalivyo katika Sheria ya Mbegu namba 18 ya mwaka 2003 na kanuni zake. Moja ya masharti hayo ni kusajiliwa na Taasisi ya kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI).

Usajili wa Wafanyabiashara wa Mbegu

Kila mfanyabiashara wa mbegu sharti asajiliwe na TOSCI kabla ya kuanza kufanya biashara ya mbegu [Sheria ya Mbegu namba 18 ya mwaka 2003 Kifungu 15 (1)]. Maombi hufanyika kupitia mfumo wa kidijitali wa eKilimo (www.portal.kilimo.go.tz) kwa wenye maduka ya mbegu, na kupitia Mfumo wa TOSCI Online Application Service (TOAS) (https://oscs.tosci.go.tz) kwa makampuni yanayozalisha au kuingiza na kutoa mbegu nje ya nchi. Aidha mtumiaji anaweza pia kuunganishwa kwenye mifumo hiyo kupitia tovuti ya taasisi (www.tosci.go.tz).

Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI atamsajili mfanyabiashara wa mbegu baada ya kujiridhisha kuwa maombi yake yamekidhi vigezo na atampatia kibali cha kumruhusu kufanya biashara ya mbegu (seed dealership certificate). Kibali hicho cha kuuza mbegu kitadumu kwa muda wa miaka 2 na baada ya hapo kinaweza kuhuishwa endapo ataomba. Kibali cha kuuza mbegu ni lazima kiwekwe wazi kwenye eneo la biashara ili wanunuzi wa mbegu pamoja na Mkaguzi wa Mbegu waweze kukiona kwa urahisi.

Mfanyabiashara aliyesajiliwa atawajibika kufuata masharti ya usajili na kama atakiuka, Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI atafuta usajili wake. Hata hivyo mfanyabishara huyo atapewa nafasi ya kujitetea kabla maamuzi ya kufuta kibali hayajafanyika. Aliyefutiwa kibali na Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI anaruhusiwa kukata rufaa kwa Waziri mwenye dhamana ya kilimo ambaye atatoa uamuzi wa mwisho. Hakuna mtu yeyote atakayeruhusiwa kuzalisha, kuingiza mbegu toka nje ya nchi, kuuza mbegu nje ya nchi, kuchakata au kusambaza na kuuza mbegu mpaka awe amesajiliwa na TOSCI na kupatiwa kibali cha kufanya biashara ya mbegu.

Mahitaji ya kujisajili kupitia mfumo wa kidijitali kwa wafanyabiashara

Ili kusajiliwa kupitia mfumo wa kidijitali, mwombaji anatakiwa kuwasilisha maombi yakiwa yameambatishwa na nyaraka zifuatazo:

  • Cheti cha mafunzo TOSCI;
  • Hati ya usajili ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN);
  • Leseni ya biashara (Pembejeo);
  • Cheti cha usajili wa Kampuni cha BRELA (Certificate of Registration);
  • Memorandum;
  • Barua pepe; na
  • Namba ya simu.

Mahitaji ili kusajiliwa kwa wafanyabiashara wadogo wa mbegu kwenye mfumo wa kidijitali

  • Hati ya usajili ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN);
  • Cheti cha mafunzo TOSCI;
  • Leseni ya biashara (Pembejeo);
  • Barua pepe na namba ya simu; na
  • Cheti cha usajili cha BRELA (Certificate of Registration) iwapo amesajili jina la Biashara.

Wajibu wa Mfanyabishara wa mbegu

Mfanyabiashara wa mbegu anao wajibu wa kufanya biashara ya mbegu kwa kuzingatia mambo yafuatayo:

  • Kuzingatia sheria ya mbegu namba 18 ya mwaka 2003 na maboresho yake pamoja na kanuni za mbegu za 2007 pamoja na maboresho yake yote.
  • Kuhifadhi nyaraka muhimu za mbegu zilizopo dukani kwake na ghalani zikionesha mafungu ya mbegu, risiti za manunuzi, hati ya mapokezi (delivery note), vyeti vya kupimwa ubora toka TOSCI na kibali cha kuingiza mbegu nchini [Kifungu cha sheria 20 (1)].
  • Mfanyabishara wa mbegu atatakiwa kumpatia mkaguzi wa mbegu nyaraka muhimu kuhusu mbegu zilizopo dukani. [Kifungu cha sheria 20 (2)].
  • Mfanyabishara wa mbegu atakayeshindwa kumpatia mkaguzi wa mbegu nyaraka muhimu za mbegu zake atakuwa amefanya kosa kisheria

Sifa za Mfanyabishara wa mbegu

  • Ni sharti awe ameidhinishwa na kusajiliwa na TOSCI katika kuendesha biashara hiyo.
  • Mmiliki au mmoja wa wafanyakazi wake katika biashara ya mbegu awe amepata mafunzo ya mbegu kutoka TOSCI (Seed dealership training).
  • Duka au ghala liwe viwango sahihi vinavyowezesha mbegu kuhifadhiwa vizuri bila kupoteza viwango vya ubora.
  • Awe na leseni ya biashara
  • Awe na Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN)
  • Awe amesajiliwa na mamlaka ya usajili kama ni kampuni, taasisi, shirika lisilo la serikali, vyama vya ushirika  au mfanyabiashara binafsi aliyesajiliwa BRELA

Baadhi ya makosa yanayofanywa na wafanyabishara wa mbegu

  • Kufanya biashara bila kusajiliwa na kupewa kibali na TOSCI
  •  Kuuza mbegu  ambazo miezi 7 imeisha toka ifanyiwe majaribio ya uotaji maabara
  •  Kutokuhifadhi rekodi ya bidhaa mbegu, risiti, delivery note n.k
  •  Kufungua vifungashio na kupima mbegu.
  • Kuweka mbegu sakafuni na siyo kwenye paleti
  •  Kuuza mbegu zisizo halali kwa mujibu wa sheria ya mbegu (Mbegu ambazo hajizaruhusiwa kuzalishwa na kuuzwa nchini)
  •  Kuuza mbegu zisizo na lebo ya TOSCI/OECD
  • Kuchanganya mbegu na bidhaa nyingine

Mambo muhimu ya kuzingatia Mfanyabiashara wa mbegu anaponunua mbegu kutoka kwenye Kampuni au Wakala Mkuu

  • Kifungashio cha mbegu kimebandikwa lebo ya ubora ya TOSCI au ya OECD Seed Schemes
  • Kifungashio cha mbegu kina taarifa muhimu kama namba ya fungu, kiwango cha uotaji na uhalisia, tarehe ya kufanyiwa majaribio ya maabara.
  • Mbegu isiwe imezidi miezi 7 toka ifanyiwe majaribio ya uotaji, au nakala za vyeti vya ubora toka TOSCI kwa mbegu ambayo imepimwa ubora kwa mara nyingine baada ya miezi 7 kupita.
  • Kuchukua risiti ya manunuzi ya mbegu na hati ya mapokezi (delivery note).