Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu

WCF Logo
Ukaguzi wa Mbegu baada ya Mavuno
Ukaguzi wa Mbegu baada ya Mavuno

Utangulizi

Ukaguzi wa maduka na maghala ya mbegu za mazao ni moja ya kazi za Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI). Katika kutekeleza kazi hiyo TOSCI huhakiki ubora wa mbegu zote zilizoko sokoni ambazo ilizithibitisha. Kwa ujumla shughuli hii ya ukaguzi hufanyika kwa kuangalia mambo makuu manne ambayo ni: (i) Usajili wa muuzaji wa mbegu (ii) Nyaraka za uthibitisho wa manunuzi ya mbegu (iii) Uthibitisho wa kutimia kwa vigezo vya ubora wa mbegu na (iv) Mazingira ya dukan a uhifadhi wa mbegu. Shughuli hii ya ukaguzi hufanyika kwa mujibu wa Sheria ya Mbegu Namba 18 ya Mwaka 2003 na Kanuni zake za Mwaka 2007 na marekebisho yake.

Wakaguzi wa Maduka na Maghala ya Mbegu

Mkaguzi wa mbegu kutoka TOSCI au Mkaguzi wa mbegu aliyedhinishwa na TOSCI ataweza kukagua duka la mbegu au stoo ya kuhifadhia mbegu (ghala) wakati wowote. Mkaguzi atapaswa kujitambulisha pindi atakapofika eneo la ukaguzi. Baada ya utambulisho mfanyabiashara wa mbegu atatakiwa kutoa ushirikiano kwa kuonesha vifuatavyo:

  1. Hati ya usajili wa mfanyabiashara wa mbegu
  2. Kuonesha nyaraka zinazohusiana na mbegu anazouza au zilizopo ghalani
  3. Kumuwezesha mkaguzi kukagua mbegu zote zilizopo dukani
  4. Kueleza na kuonesha kama kuna sehemu nyingine anakohifadhi mbegu
  5. Kusaini nyaraka za taarifa ya ukaguzi au notisi ya hatua zilizochukuliwa wakati wa ukaguzi

Mambo ya kuzingatia kwa mfanyabiashara wa Mbegu

  • Mfanyabiashara wa mbegu anapaswa kutundika Kibali cha kuuza mbegu kutoka TOSCI sehemu ya wazi dukani kwake ili kiwe rahisi kuonekana kwa wakaguzi na wanunuaji wa mbegu
  • Mfanyabiashara wa mbegu anapaswa kupokea na kuuza mbegu ambayo haijazidi miezi saba toka ipimwe ubora wake na TOSCI. Iwapo muda huo wa miezi 7 umepita tanga ipimwe, muuzaji au msambazaji anawajibika kutoa taarifa/kutuma maombi TOSCI ya kuchukuliwa sampuli kwa ajili ya majaribio ya uotaji.
  • Mfanyabiashara wa mbegu anatakiwa kuhakikisha anapatiwa nakala ya cheti cha mbegu cha maabara kutoka TOSCI ili kujiridhisha ubora wa mbegu anazozinunua iwapo zimepimwa ubora ndani ya miezi 7.
  • Mfanyabiashara wa mbegu haruhusiwi kufungua au kutoboa vifungashio vya mbegu na kuuza mbegu kwa kupima kidogokidogo, ni kosa kisheria. Utoboaji wa vifungashio upunguza nguvu ya sumu inayowekwa katika mbegu ili kulinda mbegu dhidi ya wadudu na vimelea vya magonjwa na kuruhusu unyevu kuingia na kuozesha mbegu.
  • Mfanyabiashara wa mbegu anatakiwa kumpa ushirikiano Mkaguzi wa mbegu pindi afikapo dukani kwa ukaguzi

Uwepo wa Nyaraka za Manunuzi ya Mbegu

Mbegu iliyopokelewa kutoka kwa msambazaji ili kuuzwa katika duka la mbegu husika inatakiwa kuambatanishwa na nyaraka za manunuzi, na nyaraka hizo zinatakiwa kutunzwa na kumwonesha mkaguzi wa mbegu pindi anapokagua duka hilo. Nyaraka hizo zinatakiwa kuonesha aina na kiwango cha mbegu zilizonunuliwa, jina la mnunuzi na tarehe ya kupokelewa kwa hiyo mbegu. Nyaraka hizo zinajumuhisha:

  • Risiti ya Manunuzi
  • Invoice
  • Hati ya Mapokezi
  • Kibali cha Kuingiza Mbegu Nchini na
  • Nakala ya cheti cha Ubora wa Mbegu cha TOSCI

Ni kosa kisheria kuwa na mbegu dukani bila kuwa na nyaraka tajwa hapo juu.

Lebo za Ubora wa Mbegu

Mfanyabiashara haruhusiwi kununua wala kuuza mbegu zisizo na lebo za ubora za TOSCI au za Skimu za Mbegu za OECD.

Zuio la Kuuza Mbegu

Iwapo patajitokeza kosa au mapungufu katika biashara ya mbegu zuio au faini inaweza kutolewa kwa mujibu wa sheria. Mfanyabiashara hataruhusiwa kuuza wala kuficha mbegu itakayozuiliwa mpaka atakapoelezwa hatua inayotakiwa kufanyika kutoka TOSCI kama itakavyokuwa imebainishwa katika zuio hilo.

Usafi wa Mazingira ya Ndani na Nje ya Maduka na Maghala

Sharti maduka na maghala ya mbegu yawe safi ndani na nje.

Taarifa ya Ukaguzi wa Maduka na Ghala za Mbegu

Mkaguzi wa mbegu atatoa ripoti kutokana na ukaguzi alioufanya.